Rais Samia Suluhu Hassan amesema kiongozi anatakiwa kuwa mti wa kivuli ambapo wananchi wenye shida na uhitaji wanamwendea na kupata utatuzi wa masuala yao.
Amesema hayo wakati akihutubia katika Kongamano la Wanawake wa Kiislamu Zanzibar, ambapo ametumia jukwaa hilo kusisitiza umuhimu wa wananchi kuwaheshimu viongozi wao katika ngazi zote, pamoja na kueleza wajibu na sifa za viongozi wanaotakiwa.
Amesisitiza kuwa ni muhimu wananchi kuheshimu viongozi wao, sio tu wa kisiasa, hata wa dini, hata kama wanatoka kwenye kundi dogo ndani ya jamii kwani Mungu aliona kitu ndani yao ndiyo sababu akawapa dhamana ya uongozi.
“Na sisi viongozi tunao wajibu wa kuendelea kuishi katika misingi ya uongozi bora, tunatakiwa kuwa waadilifu […] tuwe sadiki na tuwe weledi,” amesema Rais akisisitiza kuwa kiongozi anatakiwa kuwa na kauli moja atakayoisimamia, sio leo anasema hiki, kesho anabadili na kusema kingine.
Amesema viongozi wakiwa na sifa hizo, wananchi na wanaowafuata watawaheshimu na kuendelea kuwaamini.
From tbc.co.tz